IKIWA ni siku nne tangu kutokea kwa milipuko katika kambi ya Jeshi ya Gongo la Mboto, wasanii pamoja na wadau mbalimbali wa sanaa wameendelea kutoa maoni yao kuhusiana na tukio hilo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasanii na
wadau hao walilielezea tukio hili kuwa ni janga kubwa la kitaifa lililowaweka raia wengi katika hali ya huzuni na simanzi.
Aidha, walishauri serikali kupitia wizara yenye dhamana, kusoma alama za nyakati kutokana na kuwa, kambi za Jeshi ni nyingi jijini Dar es Salaam, ambazo zote zipo karibu kabisa na maeneo wanayoishi wananchi.
“Unajua, kwa mfano pale Lugalo, ile ni kambi kubwa, ni vema wananchi tungehakikishiwa usalama wetu ama kushauriwa mapema cha kufanya kabla hayajajiri maafa,” alisema Haji Mohammed, Mkurugenzi Mkuu wa kundi la mipasho la East African Melody.
Aidha, Mohammed alisema kuwa, serikali ingepanga taratibu za kuwakinga raia dhidi ya lolote linaloweza kutokea katika kambi zilizosalia, ambazo bado hazijalipuka kutokana na kuwa, chanzo cha milipuko hiyo bado hakiko wazi.
Mdau mwingine wa muziki na filamu, Mohammed Mtwale, alisema kuwa jambo la msingi kwa serikali ni kuhakikisha wanakagua maghala ya silaha mara kwa mara, ili kuwaepusha wananchi na madhara kama haya ya kulipukiwa kila baada ya muda.Na Elias Charless.
No comments:
Post a Comment