Bongo Move Chaliiiiiiiiiii

BAADHI ya mastaa wa kike wa Kiwanda cha filamu za Kibongo wamejikuta wakiangua vilio vilivyofananishwa na msiba mzito ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufuatia timu yao kutandikwa mabao 2-0 na wapinzani wao wa jadi, Bongo Flava FC kwenye tamasha la kuchangia waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto.
 

                                         
                                                  Wasanii waliokumbwa na ‘maombolezo’ hayo ni Jacqueline Steven Pentzel ‘Jack wa Chuz’ (pichani), Coletha Raymond ‘Koletha’ na  Suzan Lewis ‘Natasha’.

Walianza kuonesha sura za kupoteza matumaini baada ya timu yao ya Bongo Movie FC kukosa penalti mbili walizopewa na mwamuzi wa mchezo huo, Othman Kazi.

 Jack wa Chuz ndiye aliyepaza sauti kuangua kilio kikubwa huku akibembelezwa na mlimbwende aliyejitosa kwenye filamu, Wema Abraham Sepetu ambaye naye machozi yalikuwa yakimbubujika.

Koletha na Natasha wao walilia kwa staili ya kugugumia kitendo ambacho kiliwaacha hoi mashabiki waliofurika uwanjani hapo siku hiyo.

 Hata hivyo, baadhi ya mashabiki waliwapoza wasanii hao kwa kuwaambia kwamba, mechi hiyo ni ya kirafiki tu isiwaumize kiasi hicho.

“Unajua mechi hii ni ya  kirafiki tu jamani iweje muumie kama vile kuna kilio? Ni hali ya kawaida katika mchezo,” alisema shabiki mmoja aliyekuwa karibu na wasanii hao.

 Nilimfata Jack wa Chuz na kumuuliza kulikoni aangushe kilio uwanjani ambapo alijibu:
“Unajua nini, kitendo cha wachezaji wetu kukosa penalti mbili kimeniumiza sana, nashindwa kabisa kujizuia.”

Kwa upande wake, Koletha alisema kuwa amejikuta machozi yakimchuruzika kutokana na walivyokuwa wamejipanga katika mechi hiyo ambayo aliamini Bongo Movie FC walipania kuibuka kidedea.

 Unajua nilipoona muda umekwenda nikapoteza matumaini ya kurudisha mabao, ndipo nguvu ziliponiishia na kuanza kulia,” alisema Koletha.


                                  Baadhi ya wasanii wengine waliokuwa katika hali ya majonzi ni pamoja na Yvonne Cherly Ngatikwa ‘Monalisa’, Aunt Ezekiel, Flora Mvungi na Zuwena Mohamed ‘Shilole.’
                                             
                                                   
                                                  
                                                 
                                                 
                                                              

No comments:

Post a Comment