WAKATI maelfu ya Watanzania wakisherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya wa 2011, hali ni tete kwa msanii wa tasnia ya filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ baada ya kuumbuliwa kuhusu elimu yake na mtangazaji wa kipindi cha Leo Tena (Muvi Leo)cha Clouds FM ya Jijini Dar es Salaam, Zamaradi Mketema.
Katika mahojiano kupitia kipindi hicho kinachorushwa hewani Jumatatu hadi Ijumaa, mambo yalianza kwa Zamaradi kumuuliza Lulu kuhusu mikakati yake ya kujiendeleza kielimu.
Aidha, alimuuliza pia skendo zake mbalimbali ikiwemo ya kupiga picha ya utupu na kuiweka kwenye mtandao wa ‘Facebook’ ambapo nyota huyo wa muvi za Bongo alikanusha kwamba, picha ya utupu siyo yake na suala la shule kwake siyo ishu kwani amehitimu kidato cha nne.
“Aaa! Nimehitimu kidato cha nne mwaka huu (2010), bado nasubiri matokeo, naamini nitaendelea kidato cha tano. Kuhusu picha ya utupu ambayo inazagaa kwenye Facebook siyo yangu. Mimi nina kialama cheusi usoni ile picha ukiiangalia kwa umakini utaona haina alama hiyo,”alisema Lulu katika mahojiano hayo.
Baada ya kumaliza kumsikiliza, Zamaradi pale pale alimtwangia simu Mkuu wa Shule ya Sekondari aliyosoma msanii huyo ya St. Mary’s iliyopo Mbezi Jijini Dar aliyefahamika kwa jina moja la Otieno na kumuuliza kuhusu mwanafunzi wake huyo.
“Tunamtambua Lulu kama mwanafunzi wetu wa kidato cha tatu. Kuhusu kuhitimu kidato cha nne hatutambui kwani hajamaliza, ana muhula mzima hajahudhuria masomo. Tulimuita mama yake lakini alishindwa kuongea akapatwa na msongo (stress),” alisema Otieno.
Akaongeza: “Baadaye alikuja mjomba ‘ake (Lulu) tukazungumza naye, alipoondoka hawakuonekana tena.
“Mimi nadhani baada ya kutoka ile skendo ya picha za nusu utupu kwenye gazeti zikimuonesha amelewa aliona aibu kuja shuleni. Sisi hatujamfukuza,” alisema.
Historia fupi ya msanii huyu, alizaliwa tarehe Aprili 17, 1993 Jijini Dar. Ameibukia katika tasnia ya filamu akitokea Kundi la Sanaa la Kaole lenye makazi yake Dar. Mtu wa kwanza kumpeleka Lulu kwenye kundi hilo ni msanii Muhsein Awadh ‘Dokta Cheni’.
Wakati huo huo, Lulu amekanusha kuwa na ukaribu na mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni ‘Faza Krismasi’ wake ambaye alipigwa naye picha kwenye Shindano la kumsaka Unique Model wa Giraffe lililofanyika Desemba 24, mwaka jana.
Akiongea na mwandishi wetu jijini Dar Jumatano, Lulu alisema kuwa, mtu huyo aliyedaiwa ni ‘Faza Krismasi’ wake hamjui na ilikuwa mara yake ya kwanza kumuona ndani ya ukumbi wa hoteli hiyo iliyoko Mbezi Beach, Jijini Dar.
“Mimi simfahamu yule mliyesema Faza Krismasi wangu, ndiyo kwanza nilimuona siku ile ukumbini Giraffe, nilikaa naye karibu kwa sababu kulikuwa na kiti kiko wazi,” alisema Lulu.
Katika Gazeti la Ijumaa Wikienda, toleo la Jumatatu Desemba 27, mwaka jana ukurasa wa nyuma iliandikwa habari yenye kichwa; Lulu anaswa na Faza Krismasi wake. Hata hivyo katika habari hiyo, haikusemwa kama Lulu na mtu huyo wana uhusiano usiofaa.
No comments:
Post a Comment